Preloader

About Consolata Parish - Manda

PAROKIA YA MANDA,
JIMBO LA DODOMA,
S.L.P. 4034,
DODOMA.
HISTORIA YA PAROKIA YA MANDA.
1. UTANGULIZI
Kigango cha Manda kilianzishwa mnamo mwaka 1973 kikiwa na waamini wawili; nao ni mzee Simon Ndubaa na Joseph Charles pamoja na familia zao. Mzee simon na mkewe na watoto wawili na bwana Joseph na mkewe na mtoto mmoja.
Mzee Simon Ndubaa alikuwa anajishughulisha na kilimo na ufugaji. Bwana Joseph Charles alikuwa anajihusisha na uvuvi wa samaki kwenye bwawa la Manda.
Siku moja mzee Simon Ndubaa alikwenda kwa bwana Joseph Charles kwa ajili ya kununua samaki wa mboga. Alipofika ndani sebuleni kwa Joseph Charles akaona vitabu vikubwa mezani. Vitabu hivyo vilikuwa 5. Aina ya vitabu hivyo ni misale ya waamini, chuo kidogo cha sala, katekism, Biblia na kitabu cha historia ya kanisa. Mzee Simon akaomba asome vitabu vile kwa haraka kwa ajili ya kuokoa muda. Baada ya kuvisoma mzee Simon akamwuliza bwana Joseph, je, ulikuwa mwalimu wa dini? Akamjibu, ‘‘ndio huko kwetu Songea isipokuwa shughuli za kimaisha zimenisababishia kuacha’’. Mzee Simon akamshauri bwana Joseph, unaonaje tuanzishe kanisa? Kwa wakati huo kijiji cha Manda kilikuwa na takriban nyumba kumi. Jumapili iliyofuata basi wakaanza kusali pamoja na familia zao.
Jumapili iliyofuata walifanikiwa kufanya ibada wakiwa nyumbani kwa bwana Joseph akiongoza kama mwalimu. Waliendelea kufanya hivyo kila jumapili kwa muda wa miezi minne bila ya kupata waamini wengine lakini hawakukata tamaa.
Siku moja wakajadiliana kwamba bwana Joseph Charles aende Parokia ya Sanza (Jimbo la Singida). Hiyo ndo’ ilikuwa parokia ya karibu wakati huo. Lengo lilikuwa kumwona padre ili walau awe anafika Manda kutoa huduma za kiroho hata ingawa waamini walikuwa wachache. Alipofika Sanza aliwakuta mapadre Roland na Francesco. Akawaelezea shida yake. Pd. Roland alikubali kuwa atafika Manda atakapokwenda Ilangali(kwa sasa ni kigango cha parokia ya Manda) kuadhimisha misa. Wakati huo kigango Cha Ilangali kilikuwa kikihudumiwa na parokia ya Sanza.
Ilipofika ratiba ya kusoma misa Ilangali baada ya misa Pd. Roland alifika Manda saa 5 za asubuhi. Aliwakuta hao waamini wawili na familia zao wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa bwana Joseph Charles. Padre aliadhimisha Misa Manda kwa mara ya kwanza. Aliwapongeza hao wanafamilia na akawatia moyo kwamba waendelee wasikate tamaa. Akatoa msemo wa kuwajenga ki-imani kuwa “mkusanyikapo wawili katikati Mungu yupo”. Kumbukeni mfano wa Nuhu, waliokolewa watu wachache katika wengi.
Pd. Roland alirudi Sanza akiwa na furaha kisha akatoa agizo kuwa tarehe ya kikao cha makatekista bwana Joseph Charles ahudhurie parokiani Sanza.
Waamini walizidi kuongezeka siku hadi siku. Inaonekana wazi kwamba ziara hiyo ya kwanza ya Pd. Roland ilikuwa chachu kwa watu wa Manda.
Mwaka 1975 Pd. Roland aliendelea kutoa huduma bila kukata tamaa. Alianzisha mradi wa ufugaji wa nguruwe kwa mwalimu Joseph Charles. Baadaye alitoa agizo kwamba mwalimu Joseph aanze kufundisha mafundisho ya dini kwa wakatekumeni kwa ajili ya sakramenti ya Ubatizo na Ndoa.
Baada ya waamini kuongezeka Pd. Roland alitoa ushauri wa kujenga kanisa angalau la miti na ujenzi huo ufanywe kati ya makazi ya watu. Mwezi wa 7, 1976 jengo lilikamilika. Waamini Wahamiaji kutoka kijiji cha Mkwambe jimbo la Iringa, waliongezeka, jengo likawa dogo. Padre Roland akashauri kujenga kanisa kubwa mwaka 1978 mwezi wa 7. Padre alikuja na kuhamasisha mafundisho ya dini na kuahidi ataanza kufanya Ubatizo muda wowote.
Mwaka wa 1979 kabla ya Pd. Roland hajatoa Sakramenti ya Ubatizo na Ndoa ikatokea kuja kwa padre mwingine kutoka parokia ya Mlowa bila ya taarifa. Ikagongwa kengele ya kanisa. Ilikuwa siku ya Jumapili. Padre huyo mgeni akasoma misa, baada ya Misa kuisha akatueleza kwamba kuanzia wakati huo atakuwa padre wetu na atatoa huduma za kiroho badala ya Pd. Roland na kwamba amekuja kwa mujibu wa jimbo la Dodoma na kwamba ametumwa kuwataarifu watakuwa wanaparokia ya Mlowa. Tangia pale tukawa parokia ya Mlowa ambayo ilikuwa inahudumwa na Mapadre wa Passionists. Vigango vya Manda na Ilangali Pd. Plasido alifanya ziara mara tatu na kutoa Ubatizo kwa wakatekumeni aliowaacha Pd. Roland.
Mwaka 1980 katekista Joseph Charles akajiuzulu na nafasi yake ikachukuliwa na Simon   Lusega.
Pd. Plasido alikuta tukiwa tunasali katika kanisa la miti. Akashauri tujenge kanisa la kuta za tofali za udongo. Alituahidi atatoa bati, madirisha, mlango pamoja na ufundi. Sisi tukawajibika kufyatua tofali mwaka huo wa 1980. Tulifanikiwa kujenga mwaka huo wa 1980. Pd. Plasido alihamasisha mafundisho ya dini wajiunge wakatekumeni vijana na watu wazima wafunge ndoa. Utekelezaji wa hayo ulianza mara moja. Kanisa liliendelea kukua siku hadi siku.
Mnamo tarehe 12.10.1999, kigango cha Manda kilihamia kutoka parokia ya Mlowa na kujiunga na parokia ya Mpwayungu jimbo kuu la Dodoma chini ya baba askofu Matthias Isaya na paroko Alexy Iyulu. Wakati tukihama parokia ya Mlowa kwenda Mpwayungu tulikuwa na masharti ya kuchangia huduma katika parokia mpya kwamba kanisa lijitegemee kwa maana mapadre wahudumiwe na walei. Jambo hilo liliwafanya waamini wengi wakate tamaa. Utaratibu ulikuwa kwamba ili kupata misa lazima kuchangia mafuta ya gari la padre pamoja na michango mingine ya kulitegemeza kanisa. Hali hii ilisababisha familia nyingi kuacha kusali na zaidi zilibaki familia 6 tu zilizoendelea kubaki zikisali huku wakiongozwa na katekista Petro Katoto Michael. Hali hii iliwapelekea waamini wengine kutafuta huduma za kiroho nje ya parokia ya Mpwayungu.
Mwaka 2001 waamini wachache waliamua kufanya ujenzi wa kanisa jipya la kudumu kwa kutumia matofali ya kuchoma. Walifyatua tofali 3000 huku wakichangishana michango ya kujenga. Mchango huo ulilenga kila mwanajamii bila kujali dini, dhehebu au kabila.
Tulifanikiwa kupata fedha ya kuanzia kununua mifuko saba ya sementi. Mwaka uliofuata 2002 tulianza ujenzi.
2. KUINGIA KWA PD. ANTHONY ZANETE MANDA
Padre huyu aliingia Manda mnamo mwezi wa Agosti 2003 akitokea parokia ya Sanza; Jimbo la Singida. Alikuwa akifika maeneo ya Fuwila kama Jumuiya ndogo ndogo za kikristo kutoa huduma za kiroho. Baadhi ya wakristo wa kigango cha Manda walikuwa wakilima maeneo ya Fuwila. Waliporudi Manda walikuja kutoa taarifa kwa waamini wengine. Wakaona ni vyema wakamwombe ili awe pia anafika Manda kutoa huduma. Padre Zanete alikubali ombi hilo. Lakini akawaelekeza kwamba waandike barua kwa askofu kuomba ili wawe wanapata huduma ya kichungaji kutoka parokia ya Sanza. Barua ilipofikishwa kwa askofu, majibu yalikuwa ndiyo. Kwa hiyo Pd. Zanette akaendelea kutoa huduma katika kigango cha Manda. Tulikuwa tumeshaanza ujenzi wa kanisa kwa ugumu. Pd. Zanete akatusaidia kuikamilisha. Ujenzi ulikamilika 23.12.2006.

3. NDOTO ZA KUIFANYA MANDA KUWA PAROKIA
Ilikuwa katika ziara zake (Pd. Anthony Zanete) za uchungaji, ikiwa imefika miaka 3, mwaka 2006 bado akaendelea kutoka Sanza. Muda mwingine alikuwa akilala njiani Mtukula na Fuwila. Kutoka Manda hadi Sanza kulikuwa na umbali wa kilomita 60. Baadhi ya waamini wakamshauri padre kama ingewezekana ifunguliwe parokia ukanda huu wa Manda. Alilipokea shauri hilo na kuanza kulifanyia kazi. Wenyeji pia walimsadia kuchora ramani ya parokia mpya ya Manda ikiwa na vigango 14.
4. KUBARIKI ENEO LA UJENZI
Mwaka 2006 Baba Askofu Yuda Tadei Rwaich alibariki eneo la kujenga parokia ya Manda.
Zoezi la ujenzi lilianza kwa kufyatua tofali. Tofali zilifwatuliwa kwa malipo kutoka kwa Pd. Anthony Zanete. Baada ya tofali za mwanzo kukamilika ujenzi ulianza kwa kujenga nyumba ndogo ya kufikia wageni. Wakati ujenzi huo unaendelea, padre alikuwa amepewa malazi kwa mlei mmoja bwana Julius Sanyagoro. Yeye pia aliteuliwa na padre kusimamia ufyatuaji wa tofali. Baada ya hiyo nyumba ya wageni kukamilika, padre alihamia huko. Zoezi lililofuata ni ujenzi wa nyumba ya mapadre, na ukumbi na mabweni. Majengo hayo yalipokamilika walimwomba baba askofu kuja kuweka jiwe la msingi. Jiwe la msingi liliwekwa mnamo tarehe 28.9.2007 na Baba Askofu Yuda Tadei Rwaich.
Gharama zote za ujenzi wa majengo yote tajwa, zilitolewa na Pd. Anthony Zanete chini ya shirika la Consolata. Badaye ujenzi wa karakana ulifuata na ndipo ujenzi wa majengo mengine ukafuata.
5. KUFANYIKA UFUNGUZI WA PAROKIA
Tukio la uzinduzi wa parokia ulifanyika tarehe 21.7.2010. Parokia ilizinduliwa na Baba Askofu Yuda Thadeus Rwaich. Pd. Anthony zanete aliteuliwa kuwa paroko wa kwanza wa parokia mpya ya Manda.
Baada ya uzinduzi ujenzi pia uliendelea. Nyumba mpya ya mapadre pamoja na nyumba ya masister zilijengwa. Baada ya nyumba ya masister kukamilika, Shirika la masister wa Consolata liliwatuma masister 3; Sr. Alifya, Sr. Claudia na Sr. Elizabeth. Masister hawa walifika Manda 23.9.2011. Masister hawa walishirikiana na Pd. Zanete katika shughuli za utume katika parokia ya Manda.


6. HUDUMA MBALIMBALI ZINAZOENDELEA KUTOLEWA KATIKA PAROKIA YA MANDA
Kwanza mapadre na masister wamejijengea msingi wa Imani, na kuamasisha jamii ya waamini kuusikia ujumbe wa Mungu na kubadilika na kumjua Mungu. Pili idadi ya waamini wakatoliki wameongezeka kwa kasi kutoka familia ya watu sita mpaka familia kubwa ya Mungu. Waamini wengi wanazidi kupokea Sakramenti.
7. HUDUMA ZA KIJAMII
 Elimu kwa watoto wa chekechea inapatikana .
 Maji ikiwemo visima 7 katika vigango mbalimbali.
 Kuwasaidia wasiojiweza; hata kuwajengea nyumba.

8. MAMBO MAKUBWA YASIYOWEZA KUSAHAULIKA KWA BABA ANTHONY ZANETE
Baba Anthony Zaneth tuna mengi ya kumuelezea na sisi tunajivunia kwamba Mungu amemtumia ili tupate faraja. Tunamkumbuka kama mmisionari wa pekee kabisa na ni ushuhuda kwetu wana parokia ya Manda. Baba huyu ametufanikishia mambo ya kiroho na kimwili katika utume wake. Tunamfananisha na mchungaji mwema ambaye katika mawindo yake alikuta kundi la kondoo porini waliopotea akawakusanya na kuwarudisha nyumbani; wasiotambuliwa na mwenye mali, kisha akawatunza na kuwalinda w

MISSION GALLERY