About St. Paul Parish- Ubungo Msewe
Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume Ubungo Msewe ilikuwa ni kigango cha parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda Magomeni. Kigango hiki kilianzishwa mnamo mwaka 1968 na aliyekuwa Paroko wa Magomeni Padre Oswin wa shirika la waKapuchini. Alikihudumia kigango hicho kuanzia mwaka huo wakisaidiana na mapadre wa Chuo Kikuu. Katika kipindi hicho palikuwa waamini wachache na walisali chini ya mkorosho na baadae kujenga kibanda cha miti. Kwa msaada wa Chief Kunambi (marehemu) aliwasiliana na Balozi Richard Wambura, ambaye alitoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kanisa. Mwadhama Lauriani Rugambwa, Kardinali (marehemu) aliwakaribisha shirika la kimisionari la Consolata kuanza kuhudumu. Ndipo walianza ujenzi wa jengo la kanisa ambalo kwa sasa ndio ukumbi ndogo wa Parokia.
Mnamo tarehe 18 Machi 1973, kigango cha Msewe kulipewa hadhi ya kuwa Parokia. Na Paroko wa kwanza alikuwa Padre Igino Lumetti akisaidiwa na Padre Romano Motter. Halmashauri ya walei ya kwanza parokia ya Msewe iliongozwa na Chief Kunambi. Kwa ushirikiano na mapadre, walijenga nyumba ya mapadre ambayo hadi sasa ndimo mapadre wanaishi.
Kutokana na ukubwa wa eneo la kuhudumu, ambalo lilikuwa hadi Mbezi, vilizaliwa vigango kuwarahisishia watu kupata huduma. Mnamo tarehe 1 February 1973, kigango cha Mavurunza kilianzishwa na huduma ikaanza kutolewa na Padre Mario Biestra.
Kanisa la sasa lilianza kujengwa tarehe 9 Agost 1976 na kutabarukiwa na muadhama Lauriani Rugambwa Kardinali tarehe 15 February 1978. Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi shirika la Consolata, viongozi wa serikali wakiongozwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere (marehemu) mnamo tarehe 19 Julai 1978, Padre Romano Motter aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Ubungo Msewe. Mnamo tarehe 28 December 1980 kigango cha Makoka na Makabe vilibarikiwa . na tarehe 29 Aprili 1984 kigango cha Mbezi Luis kilibarikiwa.
Mnamo tarehe 23 Februari 1983 Padre Ricardo Ossola aliletwa Parokia ya Ubungo Msewe kuwa Paroko msaidizi kwa hiyo iliwezesha kwa kigango cha Mavurunza kupata huduma.
Mnamo tarehe 9 Septemba 2003 kigango cha Baruti kilizinduliwa. Mnamo tarehe 6 Julai 2012 Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa alitabaruku Altare ya kigango cha Baruti mnamo tarehe 6 Januari 2017 muadhama Polycarp Kardinali Pengo alitangaza kigango cha Baruti kuwa Parokia teule, na kukitanaza kuwa parokia kamili tarehe 7 Julai 2018.
Kwa sasa Parokia ya Ubungo Msewe ina kigango kimoja tu cha Mwenye heri Sr Irene Stefani-Golani. Kigango hicho kilizinduliwa tarehe 28 Agosti 2011. Kwa sasa waamini wanaendelea kumalizia ujenzi wa kanisa na mazingira yake.
Parokia ya Ubungo Msewe ina jumla ya kanda (5) tano, na jumla ya jumuiya ndongo ndogo 39 zenye waamini wapatao 3,598 na familia 814 (kwa mujibu wa sensa ya wakatoliki ya mwaka 2016) katika parokia ya Ubungo Msewe. Aidha mnamo tarehe 12 Mei 2002 tulibarikiwa na ujio wa masista wa shirika la Moyo Safi wa Bikira Maria kutoka India, wakiwa na makao yao makuu ya kanda huko Kenya, kwa sasa wanaendesha kituo cha Afya na shule ya awali na msingi.
Mnamo mwaka 1986 Padre Luciano Scaccia aliletwa kuwa Paroko wa Parokia ya Ubungo Msewe. Katika kipindi chake kama Parokia aliwezesha kujenga jingo la Allamano ambamo upo ukumbi ambao unaweza kupokea watu mia mbili na hamsini (250) kama ni sherehe na zaidi ya watu 500 kama ni mkutano wa kawaida. Na ndani ya jengo hilo kuna ofisi za parokia na kumbi ndogo za mikutano ya watu wachache, mafundisho ya sakramenti.
Tunawashukuru watangulizi wetu waliotengeneza mazingira ili parokia yetu ifike hapa ilipo. Walifanya kilichowastahili kipindi chao, sasa ni kipindi chetu kufanya juhudi zetu na kuacha alama kwa ajili ya wale wajao.
Umisionari Msewe, tukuze Imani na tuendeleze parokia.
